Sambamba na kutoa tathimini ya mafanikio na maendeleo ya kimsingi na makubwa liliyopata taifa la Iran katika mwaka uliopita wa 1391 Hijria Shamsia licha ya kuweko vizuizi vingi na vikubwa sana vya kivitendo na kipropaganda vya watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran, ametolea ufafanuzi nukta kadhaa za kimsingi kuhusu mazungumzo na Marekani na pia masuala ya lazima na yanayohitajika katika hamasa ya kiuchumi na hususan wajibu wa kuacha kutegemea mafuta katika bajeti ya nchi na kuzipa mazingatio makubwa siasa kuu za kiuchumi pamoja na kuchukua hatua za kiwerevu kabla adui hajatekeleza njama zake. Vile vile alizungumzia mambo ya lazima katika hamasa ya kisiasa na hasa hasa kushiriki vilivyo wananchi katika uchaguzi wa mwaka huu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, katika uchaguzi huo inabidi watu wa mitazamo na mawazo tofauti na wa mirengo mbali mbali ambao ni wafuasi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, washiriki kwenye uchaguzi huo na kwa taufiki ya Mwenyezi Mungu na hima ya wananchi wa Iran kuweze kushuhudiwa uchaguzi wa kufana kwani uchaguzi wa Rais una athari kubwa katika masuala yote makuu ya nchi. Ayatullah Udhma Sayyid Khamenei alianza hotuba yake kwa kutoa mkono wa baraka kwa mara nyingine tena kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Hijria Shamsia na baadaye kutoa tathmini juu ya nukta chanya na nukta dhaifu zilizoshuhudiwa nchini Iran katika mwaka uliopita na kusisitiza kuwa ni jambo la dharura kuwa na mipangilio mizuri kwa kutegemea msingi wa tathmini hiyo kuu. Aliongeza kuwa: Kama ambavyo mtu anahitajika mara zote kutathmini na kuchunguza masuala yake ya kila siku, ni vivyo hivyo katika masuala ya nchi, kunahitajika tathmini na ukadirifu wa kitafa na hilo ni jambo muhimu sana kwani linatoa ibra na funzo na kuonesha njia ya kufuata katika masuala yaliyopo na yanayokuja. Vile vile akaashiria jinsi mataifa, wasomi na watu muhimu wa nchi mbali mbali wanavyoangalia kwa kina kazi na mafanikio ya taifa la Iran ili waweze kupata somo na kigezo cha kufuata, na namna maadui wanavyoangalia kwa kina mafanikio ya taifa la Iran na baadhi ya wakati udhaifu unaojitokeza kwa taifa hilo na kusisitiza kwamba: Katika upande huo pia taifa la Iran linapaswa kuwa na mtazamo mkuu na unaokubaliana na uhakika wa mambo na vile vile liwe na tathmini sahihi kuhusu hali ilivyo nchini.Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema kuwa, kutathmini hali ilivyo nchini kwa kuangalia tu masuala kama vile maisha kuwa juu, kupungua uzalishaji katika baadhi ya sekta za uzalishaji na mashinikizo ya kiuchumi, ni kupima mambo nusu nusu, si ukadirifu kamili na wala si tathmini iliyosimama juu ya uhalisia wa mambo. Alisema kwamba: Kipimo na tathmini sahihi ni kwamba, pamoja na kuweko udhaifu na matatizo katika medani hiyo adhimu iliyojaa changamoto kwa taifa la Iran, yalikuweko pia maendeleo na mafanikio makubwa na kwa kuzingatia uhakika huo tutaona kuwa, taifa la Iran limepata mafanikio makubwa na limedhihiri kifua mbele na kwa ushujaa katika medani hiyo.Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia namna Marekani inavyotoa tathmini yake waziwazi kuhusiana na kuliwekea vikwazo na mashinikizo taifa la Iran kwa kusema bila kificho kuwa vikwazo hivyo vimewekwa ili kulifanya kilema taifa la Iran na kuongeza kuwa: Katika medani hiyo iliyojaa changamoto, taifa la Iran kwa werevu wa hali ya juu na kwa nguvu zake nyingi, limefanikiwa kubadilisha vitisho hiyo kuwa fursa nzuri kwake na mfano wake ni kama mtu anayechukua ubingwa katika michezo, ambaye huibuka na ushindi baada ya kuvuuka kwenye mapambano na ushindani mkubwa ulioambatana na tabu na mashaki mengi na juhudi zisizochoka na hatimaye kupongezwa na watu wote kwa ushindi anaoupata. Ameongeza kuwa: Iwapo kipimo na tathmini ya masuala ya nchi na mazingira yake itakuwa kwa namna hiyo, bila ya shaka yoyote tutaona kuwa, bingwa wa medani hiyo adhimu ni taifa la Iran.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Mafanikio na ufanisi wa taifa la Iran katika medani hiyo iliyojaa changamoto ni mkubwa kiasi kwamba ufanisi huo hata umesifiwa na weledi wa mambo wanaoangalia mambo kwa kina na wasomi na watu muhimu na wenye ushawishi wa kisiasa katika nchi mbali mbali duniani na hata katika nchi zinazoitakia mabaya Iran.Ayatullah Udhma Khamenei aidha ameliashiria lile kundi la watu ambao daima hawafurahishwi na maendeleo ya Iran na kusisitiza kuwa, kundi hilo ambalo linaundwa na maadui wa taifa la Iran linatumia mbinu namna mbili kukabiliana na maendeleo ya Iran: 1 - Kuweka vizuizi vya kivitendo kama vile vikwazo, vitisho na kuwashughulisha viongozi, wasomi na wananchi wa Iran na masuala ya pembeni yasiyo na kipaumbele chochote, na 2 - Kufanya propaganda kubwa sana za kuficha maendeleo ya taifa la Iran ili walimwengu wasiyaone maendeleo hayo na kukuza kupindukia udhaifu unaojitokeza kwa taifa hili (ili walimwengu wahisi hakuna maendeleo yoyote ambayo taifa la Iran limeyapata).Alisema, katika upande huo, mwaka wa 1391 Hijria Shamsia ulikuwa ni mwaka wa kazi nyingi kwa watu wasiolitakia mema taifa la Iran ikilinganishwa na miaka ya kabla yake na kuongeza kuwa: Maadui wa taifa la Iran wamesema wazi kuwa, lengo lao ni kulifanya kilema na kulipigisha magoti taifa la Iran, hivyo iwapo taifa la Iran litakabiliana vilivyo na vikwazo vyote hivyo na kuendelea kuwa imara bila ya kutetereka bali na kuzidi kupata maendeleo katika nyuga tofauti, jambo hilo kwa hakika litawaaibisha maadui hao.Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza maswali mawili: 1 - Liko wapi pango kuu la njama dhidi ya taifa la Iran? 2 - Maadui wa taifa la Iran ni akina nani?Akijibu swali la kwanza, Ayatullah Udhma Khamenei akisema: Kituo kikuu cha njama dhidi ya taifa la Iran ni Marekani kiasi kwamba leo hii na baada ya kupita miaka 34 ya njama dhidi ya taifa la Iran, unapotaja neno adui tu, akili za wananchi wa Iran moja kwa moja zinalenga kwa Marekani. Ameongeza kuwa: Viongozi wa Marekani wanapaswa kutaamali na kulizingatia kwa kina suala hilo na wajiulize, kwa nini akili ya taifa la Iran kuhusu adui wakati wote inalenga moja kwa moja kwa Marekani? Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu vile vile alisema kuhusu maadui wa taifa la Iran kwamba: Mbali na Marekani ambaye ni adui nambari moja na ni kituo kikuu cha njama dhidi ya Iran, kuna na maadui wengineo ambapo serikali khabithi ya Uingereza ni miongoni mwa maadui hao, lakini Uingereza yenyewe haina uhuru, bali inafuata mkumbo, ni mkamilishaji tu wa njama za Marekani.Aidha katika sehemu hiyo ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei ameitahadharisha serikali ya Ufaransa na kusema kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa na tatizo na serikali na wala taifa la Ufaransa, lakini serikali ya Ufaransa katika miaka ya hivi karibuni na hasa hasa wakati wa utawala wa Sarkozy imekuwa ikifuata siasa za uadui wa wazi wazi dhidi ya taifa la Iran. Lakini serikali ya Ufaransa inapaswa kujua kuwa, siasa hizo ni ghalati na ni kosa kubwa kuendelea nazo, si siasa za kimantiki, bali watu wenye busara na akili, hawamfanyi mtu ambaye si adui yao kuwa adui yao.Vile vile ameuashiria utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema kuwa: Utawala ghasibu wa Kizayuni hata hauko katika daraja na hadhi ya kuwa adui wa taifa la Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aligusia baadhi ya vitisho vinavyotolewa na viongozi wa utawala wa Kizayuni vya kudai kuwa vitaishambulia kijeshi Iran na kusisitiza kwamba: Kama Israel (Wazayuni) itathubutu kufanya kosa lolote lile kuishambulia Iran, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Kiislamu ya Iran itaifutilia Tel Aviv na kuisawazisha na ardhi mara moja.Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Daima utawasikia Wamarekani wanawatumia maadui hao wachache wa taifa la Iran na kuwapa jina lisilo sahihi. Wanaziita nchi hizo "Jamii ya Kimataifa" wakati ambapo "Jamii ya Kimataifa" kamwe haina uadui na Muirani na wala Iran ya Kiislamu.Baada ya kuwatangaza maadui wa kweli na wachache wa Iran, Ayatullah Udhma Khamenei ameanza kutoa ufafanuzi kuhusu hatua za kiadui zilizochukuliwa na maadui hao mwaka uliomalizika wa 1391 Hijria Shamsia na kuongeza kuwa: Tofauti na madai yao ya kujifanya ni marafiki wa taifa la Iran, Wamarekani tangu mwanzoni kabisa mwa mwaka uliopita ilishadidisha vikwazo vyake na kuiwekea Iran vikwazo vikubwa vya mafuta na Benki na hadi hivi sasa wanashikilia kuwa si maadui wa taifa la Iran licha ya kuchukua kwao hatua hizo za kiuadui.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, siasa hizo ni kuendelea na siasa zile zile za "kuficha makucha ndani ya glovu za mahameli" (siasa za kuuma na kupuliza) na kuongeza kuwa: Tofauti kabisa na madai yao ya kudanganya watu, Wamarekani walianzisha mpango maalumu uliokuwa umepangiliwa vyema dhidi ya taifa la Iran na walitaraji kuwa baada ya kupita miezi michache tu, taifa la Iran litasalimu amri na kupigia magoti siasa zao za kibeberu na litaachana na harakati zake za kujiletea maendeleo ya kielimu, lakini kilichojiri kilikuwa ni kitu tofauti kabisa na matarajio ya watu hao wasiolitakia mema taifa la Iran.Ayatullah Udhma Khamenei ameashiria pia jinsi viongozi wa Marekani walivyoshindwa kuficha furaha zao kutokana na taathira za vikwazo vyao na matamshi ya baadhi ya viongozi wa Iran kuhusu suala hilo na kuongeza kuwa: Ni kweli vikwazo hivyo vimetuathiri, lakini havikuwa na taathira iliyokusudiwa na maadui hao. Ameongeza kuwa: Kama vikwazo vimeacha athari sababu yake kuu ni kuwa uchumi wa nchi unategemea mafuta na ni kwa sababu hiyo ndio maana likawa ni jambo la wajibu kuwa na uchumi usiotegemea mafuta na hilo ndilo linalopaswa kuwa suala la kupewa kipaumbele kikuu katika mipango ya serikali ijayo.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia matamshi yake aliyoyatoa miaka kadhaa nyuma kuhusu wajibu wa kufikia katika hatua ambayo itawezekana kufunga visima vya mafuta na kuendesha nchi bila ya kutegemea hata tone moja la mafuta na kuongeza kuwa: Wakati huo baadhi ya watu ambao wenyewe wanajiita wasomi walitoa tabasamu za kejeli kuhusiana na matamshi hayo na wakasema; hivi kitu kama hicho kinawezekana kweli?Ayatullah Udhma Khamenei amesisitiza pia kuwa: Ni jambo linalowezekana kabisa kufikia kwenye uchumi usiotegemea mafuta hata kidogo, lakini jambo hilo lina masharti yake nayo ni kuwa na mipangilio sahihi.Baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu hatua za chuki zilizochukuliwa na maadui katika mwaka uliopita wa 1391 Hijria Shamsia dhidi ya taifa la Iran katika upande wa kiuchumi, ameashiria njama za maadui hao katika upande wa kisiasa na kusema kuwa: Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na watu wanaolitakia mabaya taifa la Iran katika upande wa kisiasa, ni kujaribu kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itengwe kimataifa, lakini kufanyika kikao cha wakuu wa nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini Tehran na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wakuu na viongozi wa ngazi za juu wa nchi wanachama wa harakati hiyo na kuipongeza Iran kutokana na maendeleo yake ya kustaajabisha ya kisayansi na kiteknolojia, kulifelisha kikamilifu njama hizo za maadui. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, hatua nyingine iliyochukuliwa na maadui katika mwaka uliopita ni kujaribu kuwatia wasiwasi wananchi wa Iran na kuwafanya wajiweke mbali na mfumo wao wa utawala yaani Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Kushiriki kwa wingi mno na kwa hamasa na shauku kubwa wananchi wa Iran katika maandamano ya Bahman 22 (wakati wa maadhimisho ya Mapinduzi ya Kiislamu) na kuonyesha mapenzi yao makubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu, kulitoa pigo jingine kubwa kwa maadui. Ayatullah Udhma Khamenei ametaja baadhi ya njama zilizoshindwa katika masuala ya usalama na njama za kutaka kupunguza ushawishi na nguzu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika eneo hili kuwa ni hatua nyingine za kiadui zilizochukuliwa na watu wasiolipendea mema taifa la Iran katika mwaka uliopita wa Hijria Shamsia.Ameongeza kuwa: Uwepo wa Iran yenye nguvu nyuma ya vita vya siku nane vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza huko Palestina na kwa mara ya kwanza kuweza wanamapambano wa Palestina kuupigisha magoti utawala wa Kizayuni na vile vile kukiri maadui wa Iran kuwa masuala ya Mashariki ya Kati hayawezi kutatuliwa bila ya kushirikishwa Iran ni ushahidi mwingine unaothibitisha kufeli njama za maadui katika upande huo.Vile vile amesisitiza kuwa: Mashinikio yote haya na uadui wote huu hususan vikwazo vya kila nui pamoja na kwamba vimekuwa na taathira hasi, lakini pia vimekuwa na athari kubwa chanya kwa taifa la Iran na muhimu kuliko yote ni kuwa vikwazo na mashinikizo hayo yamepelekea kupata nguvu uwezo ya ndani ya Iran na vipaji vya wananchi wa taifa hili kulikopelekea kufanikishwa kazi kubwa muhimu na za kimsingi katika mwaka uliopita.Baada ya hapo Ayatullah Udhma Khamenei amezungumzia baadhi ya maendeleo na mafanikio makubwa na ya kimsingi liliyopata taifa la Iran mwaka 1391 Hijria Shamsia licha ya kuwa chini ya mashinikizo makubwa ya maadui na kuongeza kuwa: Kupatikana vyanzo vingine vipya vya mafuta na vyanzo vingine vipya vya urani, kuanzisha na kupanua vinu na viwanda vya mafuta, kuchukuliwa hatua za kimsingi katika upande wa barabara na katika masuala ya nishati, kupatikana mafanikio makubwa ya kisayansi na kiteknolojia ikiwa ni pamoja na kutuma anga za juu satalaiti ya Nahid na satalaiti ya utafiti yenye kiumbe hai, kutengeneza ndege za kisasa kabisa za kivita, kuzalisha dawa muhimu mno zenye michanganyiko tofauti mipya na kushika nafasi za kwanza na daraja za juu katika masuala ya kielimu, kuongezeka kasi ya maendeleo ya kielimu, kuongezeka idadi ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu na wasomi wa Kiirani yote hayo ni maendeleo, ufanisi na mafanikio makubwa liliyopata taifa la Iran katika mwaka ambao maadui walikusudia kulifanya kilema taifa la Iran kupitia vikwazo vyao hivyo.Amesisitiza kuwa: Somo kubwa linalopakatikana kutokana na ufanisi na mafanikio hayo makubwa ya mwaka uliopita wa 91 ni kwamba taifa lililo hai kamwe haliwezi kupigishwa magoti na vikwazo, mashinikizo na mibinyo ya adui.Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha pia nukta dhaifu zilizoshuhudiwa katika uchumi wa Iran kwenye mwaka uliopita na kuongeza kuwa: Kitendo cha uchumi wa nchi kutegemea mafuta, kutozingatiwa siasa kuu za kiuchumi, kukumbwa na siasa zile zile za kila siku ni miongoni mwa nukta hasi ambazo viongozi nchini na hasa serikali ijayo inapaswa kuyazingatia na kuyapa uzito wa hali ya juu na ijulikane kwamba nchi hivi sasa inahitajia kuwa na siasa kuu za kiuchumi, zilizo wazi, zilizopangiliwa vizuri na zenye umakini wa hali ya juu.Pia amesema, somo jingine linalopatikana kutoka katika mwaka ulioisha wa 1391 Hijria Shamsia ni kujulikana uwezo mkubwa ilio nao Iran na kuongeza kuwa: Kadiri uwezo wa nchi unavyokuwa mkubwa na viongozi wa nchi wanapokuwa na umoja na mshikamano na kufanya kazi zao kwa umakini na tadibiri ya hali ya juu, ndivyo taathira hasi za vitendo vya kiuadui vya adui zinavyozidi kuwa ndogo sana.Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amesisitiza kwamba, mbali na masuala ya uchumi, masuala yanayohusiana na amani, usalama wa wananchi, maendeleo ya kielimu, uhuru na heshima ya taifa, nayo ni muhimu kwa nchi na kuongeza kuwa: Taifa la Iran kutokana na mafanikio liliyopata mwaka uliopita limeweza kuwathibitishia walimwengu kuwa, kutokuwa kibaraka wa Marekani na madola makubwa ya kibeberu si tu hakulifanyi taifa kubaki nyuma kimaendeleo, bali kunalifanya taifa hilo liwe huru na kupiga hatua kubwa za kimaendeleo.Baada ya kutoa tathmini jumla kuhusu hali ilivyokuwa katika mwaka ulioisha wa 91, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia nukta mbili kuhusu mustakbali au mambo ambayo yanaweza kuwa funzo kutoka katika masuala ya mwaka uliopita. Kuelewa njama za adui kabla ya kutekeleza njama zake hizo na kupambana kibusara na kwa umahiri wa hali ya juu na njama za maadui, ilikuwa ni nukta ya kwanza iliyoashiriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sehemu hiyo ya hotuba yake.Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Hatua ya wa
Hotuba ya Sayyid Ali Khamenei kwa munasaba wa mwaka mpya
Kama Israel itathubutu kuishambulia Iran, basi tutaifuta Tel Aviv na kuisawazisha ardhi mara moja/Sisi hatupingi mazungumzo na
29 Machi 2013 - 19:30
Msimbo wa Habari: 404449
Ayatullah Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, alizungumza (Alkhamisi) ambayo ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwaka mpya wa Kiirani wa 1392 Hijria Shamsia, na kutowa hotuba muhimu sana mbele ya umati mkubwa wa maelfu ya wafanyaziara na watu wanaoishi jirani na Haram takatifu ya Imam Ali bin Musa Ridha (AS) waliokuwa wakikusanyika kwenye haram hiyo.